Wanakijiji wamchoma moto kuondoa laana mwanaume anayedaiwa kumuua mkewe
Katika hali ya mshangao, mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Sylvester Matika (47) mkazi wa Kijiji cha Ibwichina, kaunti ya Kakamega nchini Kenya ameuawa kwa kuchomwa moto na wanakijiji, akituhumiwa kumuua mke wake.
Matika anadaiwa kumuua mke wake mwenye umri wa miaka 40, hali iliyoamsha hasira kali miongoni mwa wanakijiji, ambapo walimkamata mtuhumiwa huyo na kumchoma moto pamoja na kuteketeza makazi yake.
Kulingana na Vincent Arambe Lusala, mkazi wa kijiji hicho, Matika alihamia Ibwichina miaka kadhaa iliyopita, lakini kumekuwepo na uvumi kuwa alikimbia nyumbani kwao baada ya kuhusishwa na mauaji ya jamaa mwingine.
Wanakijiji hao walichukua hatua hiyo kama sehemu ya ibada ya “kutakasa eneo” kutokana na imani ya kwamba mtu anayehusishwa na mauaji ya jamaa huleta laana. “Pindi mtu anaposhukiwa kumuua jamaa yake, kuna laana, na njia pekee ya kutakasa eneo ni kuondoa mali zote za mshukiwa,” amesema Arambe Lusala.
Jeshi la polisi limeanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na limetoa onyo kwa wananchi dhidi ya kujichukulia sheria mikononi. Miili ya wawili hao imepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega kwa ajili ya uchunguzi zaidi.