Wananchi 1,386,656 wafikiwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia

0
5

Wizara ya Katiba na Sheria imeeleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa Kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, Jumla ya wananchi milioni 1,386,656 wamefikiwa kwenye mikoa 17 iliyofikiwa na kampeni hiyo, huku jumla ya migogoro 14,775 ikipokelewa na kushughulikiwa na wanasheria wanaoshiriki kwenye kampeni hiyo.

Ameyasema hayo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kwa niaba ya Waziri wa Katiba na sheria, Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo mkoani humo ambapo ameeleza kuwa katika migogoro hiyo, 2885 imesikilizwa, kutatuliwa na kuhitimishwa na mingine 11,890 inaendelea kushughulikiwa kwenye ngazi mbalimbali za kimaamuzi.

Aidha, Mtanda ameeleza kuwa kampeni hiyo imesaidia kupatikana kwa haki, msaada wa kisheria na elimu ya sheria kwa wananchi wa pembezoni pamoja na kuwafikia wananchi wasio na uwezo.

Pia amewasisitiza viongozi wa ngazi za Halmashauri za Mkoa wa Mwanza, Viongozi wa dini na wa kimila kuhamasisha wananchi kujitokeza kikamilifu kushiriki kwenye kampeni hiyo ili kupata usaidizi wa kisheria sambamba na viongozi wa serikali za mitaa ambao watakuwa na mafunzo maalum ya kukumbushwa wajibu wao na namna wanavyoweza kutatua migogoro katika maeneo yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Send this to a friend