Wananchi 36 wafika Muhimbili wakitaka kuuza figo

0
57

Hospitali ya Taifa Muhimbili imetoa ripoti ya takwimu zinazoonesha kupokea maombi ya wananchi 36 walioomba utaratibu wa kuuza figo zao ili kukabiliana na ugumu wa maisha.

Takwimu hiyo imetolewa jana wakati wa maadhimisho ya siku ya kukabiliana na ugonjwa wa Figo duniani.

Awali, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka kitengo cha figo Muhimbili, Halid Mahenga alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa kati ya Januari hadi Februari, watu sita walikwenda hospitalini hapo wakiulizia utaratibu wa kuuza figo zao.

Aidha, Mahenga katika taarifa yake kwa umma, alisema kati ya mwaka 2019 na 2020 idara yake ilipokea maombi ya watu watatu waliohitaji kupewa utaratibu wa kuuza figo zao, huku mwaka 2021 wakipokea watu wengine 27 ambao baadhi yao wamedai chanzo kuwa ni ugumu wa maisha.

Hata hivyo, ameeleza kuwa wakati serikali ikiendelea kufanyia kazi maandalizi ya sheria ya upandikizaji wa viungo, hospitali hiyo kwa sasa inaendelea kuzingatia misingi yote ya maadili kitaaluma katika upandikizaji wa figo.

“Ni muhimu watu wakatambua kwamba ni makosa kisheria, mgonjwa akihitaji upandikizaji hospitali itazingatia kanuni zinazohitajika kwa mtu anayetakiwa kuchangia figo kwa mgonjwa mwenye uhusiano wa damu” Alisema Mahenga

Hospitali ya Muhimbili tayari imepandikiza figo kwa wagonjwa 68 tangu kuanza kwa huduma hiyo nchini mwaka 2017, huku wagonjwa 110 hadi 120 wakipewa huduma ya usafishaji figo kila siku hospitalini hapo.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend