Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linawashikilia watu watano wakazi wa Kijiji cha Ilagala kata ya Ilagala wilayani Uvinza mkoani Kigoma walioshiriki kufunga barabara wakishinikiza kufanyika kwa ramli chonganishi ili kuwasaka wachawi.
Akizungumza na Swahili Times Kamanda wa Polisi mkoani humo, Philemon Makungu amesema tukio hilo limetokea Juni 17, mwaka huu ambapo wananchi wa Kijiji hicho walitaka kumsimamisha RPC wa mkoa huo ili awaruhusu kufanya shughuli hizo, na baada ya kukataliwa ombi lao ndipo fujo zilipoanza.
Aidha, Kamanda Makungu ameeleza kuwa katika hali hiyo mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa wananchi hao amefariki dunia wakati wakikabiliana na polisi, huku baadhi ya askari wakijeruhiwa, na magari matatu ya polisi yakipigwa mawe.
RC Chalamila: Wanaopanga kuandamana waache mara moja
“Kufunga barabara ni kinyume cha sheria, wao kiutaratibu wangeenda kwa viongozi watoe maoni yao ambao ni utaratibu wa kistaarabu kabisa, sasa badala yake kila kiongozi akipita unafunga barabara tena kwa shughuli za haramu? Hilo halikubaliki,” amesisitiza Kamanda Makungu.
Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwemo kutoa maoni yao kwa ustaarabu ili kuepusha vurugu.
“Wananchi wafuate sheria, mambo ya kupiga ramli chonganishi hayakubaliki kisheria, na tutahakikisha kwamba wote wanaofanya hivyo tunawaelimisha na ambaye haelimiki basi tutamfikisha mbele ya sheria. Lakini pia kama ni malalamiko hufanyi fujo, sisi hatuna shida na wewe,” amesema.