Wananchi wachoma moto nyumba ya mwenyekiti kwa madai anawaonea

0
73

Wananchi wa Kitongoji namba 2, Kata ya Mwakitolyo Wilaya ya Shinyanga wamechoma nyumba ya Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Shabani Zoro na kuvunja nyumba ya kiongozi wa Sungusungu, Buyaga Kazimoto wakiwatuhumu kuwaonea wananchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tukio la kuchoma moto nyumba za viongozi na kuharibu mali zao ni baada ya kuwatuhumu viongozi hao kuwaonea wananchi na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Mwanamke (56) adaiwa kumbaka mtoto (8), amchubua sehemu za siri

Aidha Kyando ameongeza kuwa kijana aliyeuawa anafahamika kwa jina la Jackson Joseph (35), mchimbaji mdogo wa madini, aliyepigwa risasi Mei 18, mwaka huu baada ya kujaribu kumnyang’anya bunduki mlinzi wa kampuni ya Light Ndovu Security aliyekwenda kuamua ugomvi baina ya marehemu na mke wake.

Kisa hicho kinadaiwa kutokea baada ya mke wa marehemu kuomba msaada na ndipo majirani wakapiga simu kwa kiongozi wa sungusungu ambaye naye alichukua walinzi wanne wa kampuni binafsi ya ulinzi wakiwa na silaha za moto kwenda kumkamata mwanaume huyo na kusababisha mauaji.

Amefafanua kuwa baada ya tukio hilo wananchi walishikwa na hasira na kuamua kuharibu mali zao ikiwemo kuchoma nyumba, pikipiki na kuvunja duka na ofisi ya kitongoji.

Hata hivyo, amesema jeshi linamshikilia mlinzi wa kampuni hiyo ya ulinzi, Abdul Chacha kwa tuhuma za mauaji, na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Send this to a friend