Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ikwambi kata ya Mofu, Tarafa ya Mngeta Wilaya ya Kilombero wanadaiwa kuchoma moto ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Mofu na kusababisha vifo vya watu wawili kutokana na kutoridhishwa na maamuzi yanayotolewa na viongozi wakati wa utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na Mwananchi mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Ikwambi, Victor Timbulu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana Oktoba 13 huku Diwani wa Kata ya Mofu, Greyson Mgonera akijeruhiwa vibaya maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Mzee wa miaka 70 akatwa uume na watu wasiojulikana
Ameeleza kuwa wakati viongozi wa Kijiji na Kata wakiwa kwenye kikao, wananchi walifanya maadamano hadi kwenye ofisi hiyo na kuchoma moto huku wakilalamika viongozi kuwapendelea wafugaji na kila wanapopeleka malalamiko hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
“Juzi wakulima kama kumi walipigwa na wafugaji na ilitolewa taarifa kituo kidogo cha polisi lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa,” amesema Timbulu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi amekiri kuwepo kwa tukio hilo na mpaka sasa watu tisa wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.