Wananchi waeleza kupata ahueni kwa kuimarishwa kitengo cha kusafisha damu Hospitali ya Rufaa Tanga

0
25

Wananchi wa Mkoa wa Tanga wamepata ahueni ya matibabu, baada Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga kufanyiwa maboresho yakiwemo kuanzishwa kitengo cha kusafisha damu, hatua iliyowapa unafuu kwa wagonjwa kutokwenda mbali kupatiwa matibabu.

Hapo awali  wagonjwa waliohitaji kupatiwa huduma hiyo iliwabidi wasafiri kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, ila kwasasa wanapatiwa matibabu hayo mkoani hapo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Tanga, Juma Ramadhani amesema kuwa wagonjwa waliokuwa wakifika katika hospitali hiyo hawakuweza kupewa huduma ya kusafisha damu hivyo walipewa rufaa ya kwenda  katika Muhimbili.

Mmoja wa wagonjwa kutoka Hospitalini hapo amesema hapo awali ilibidi atumie fedha nyingi kusafiri, pesa ya chakula, usafiri wa kwenda Muhimbili na kurudi na kulipia hoteli, lakini kwa sasa wamesogezewa karibu huduma hiyo.

Maboresho mengi yamefanyika toka kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa mjini hapo,  hali iliyowafanya wananchi wa Tanga kuendelea kupata huduma nyingi wanazozihitaji na kupunguza idadi kubwa ya vifo.

Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Tanga ulianzishwa mwaka 1896 na kukamilika miaka tisa baadaye, kutokana na vifo vingi vilivyosababishwa na malaria na hakukuwa na vituo bora vya afya, hivyo  wazo la kuanzishwa kwa Hospitali mjini Tanga lilizaliwa.

Send this to a friend