Wanaohama Ngorongoro kwa hiari wamshukuru Rais Samia

0
52

Baadhi ya wakazi wa Ngorongoro mkoani Arusha ambao wameamua kuhama kwa hiari kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha nao wanakuwa na makazi ya kudumu eneo la Msomera wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Wakizungumza na TBC wakati wakiezua nyumba zao tayari kwa kuhama katika eneo hilo kwa hiari, wamesema walikuwa wanaisubiri fursa hiyo kwa muda mrefu lakini Rais Samia ameitekeleza, hivyo wanamshukuru kwa uamuzi wake.

Aidha, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Beatrice Soka amesema amefurahi kuhama kwa sababu kwa muda mrefu walitamani mchakato huo ufanyike lakini ulichelewa.

“Bahati nzuri nimekwenda huko Msomera na nimerudi jana. Nimeshuhudia kwa macho yangu na akili zangu kwa kweli fursa tuliyopewa na Rais Samia ni ya kipekee, ni fursa ya upendeleo kwa wana Ngorongoro wote.”

Ameongeza kuwa “kuna shule, huduma ya maji , miundombinu yote na kuna mabwawa ya kutosha, nyumba, mzunguko wa nyumba kuna ekari tatu mbali na mashamba yalipo nje ya pale ekari tano, na mama Samia ametuwezesha tuliotoka hapa tuweze kwenda kuendelea na kasi kwani tumepoteza muda.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesema zoezi hilo ni la hiari na walioamua kuondoka wamefikia hatua hiyo baada ya kujadiliana na familia zao na kuafiki mpango huo bila kulazimishwa.

Send this to a friend