Wanasayansi wa Uingereza kukamilisha chanjo ya Corona mwezi Septemba

0
38

Wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa kukabilia na mlipuko wa virusi vya corona, wanasayansi wameeleza kuwa chanjo ya virusi hivyo inaweza kuwa imepatikana ifikapo Septemba mwaka huu.

Profesa anayehusika na chanjo kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, Sarah Gilbert amesema kuwa anauhakika kwa asilimia 80 kwamba chanjo iliyopo kwenye matayarisho itafanya kazi mwezi Septemba.

Hata hivyo baadhi ya watalaamu wametoa tahadhari kwamba chanjo huchukua zaidi ya mwaka kukamilika, na chanjo ya virusi vya corona inaweza kuchukua kati ya miezi 12 hadi 18.

Gilbert ameongeza kuwa majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu yanatarajiw akuanza ndani ya wiki mbili zijazo.

Kauli hiyo yenye matumaini ya kurejesha mfumo wa maisha ya binadamu katika hali ya kawaida imekuja wakati ambapo zaidi ya watu 115,220 wamefariki duniani kote hadi Aprili 13 mwaka huu kutokana na kuathiriwa na virusi hivyo.

Profesa huyo ameeleza kuwa kwa sasa anaendelea na mazungumzi na serikali ili iweze kufadhili shughuli hiyo na kuanza uzalishaji wa chanjo hiyo mapema hata kabla ya majibu ya hatua ya mwisho hayajatoka ili kuwawezesha watu wengi zaidi wapate pindi itakapothibitika kuwa inafanya kazi.

Ameongeza kuwa kufanikiwa kwa mchakato huo katika kipindi cha vuli kunategemea kama mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa.

Timu ya Profesa Gilbert ni miongoni mwa timu zinazoendelea na tafiti za kuja na chanjo ya kuzuia virusi hivyo vinavyosababisha homa ya mapafu.

Send this to a friend