Wanaume Katavi: Wanawake wakipata pesa wanatunyanyasa na kutunyima tendo la ndoa

0
65

Wanaume wa Kijiji cha Mapili Halmashauri ya Milele mkoani Katavi wamesema wanashindwa kuwawezesha kiuchumi wake zao wakihofia wanawake wao kubadilika ikiwa ni pamoja na kutowasikiliza na wengine wakidai kunyimwa tendo la ndoa.

Hayo yamezungumzwa kijijini hapo katika mdahalo maalum ulioandaliwa na Shirika lisilo la Serikali la Marie Stopez Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu ya afya ya uzazi na masuala ya ukatili wa kijinsia.

Mmoja kati ya wanaume wa kijiji hicho, Juma Kapangano ameeleza kuwa wake zao huwanyanyasa na kujiona wapo juu ya waume zao pindi wanapopata pesa.

“Sisi wanaume sio wanyanyasaji isipokuwa wake zetu ndio hutunyanyasa, kwa sababu utakuta mtu unampa mtaji halafu baadaye anakuja kukugeuka,” amesema Kapangano.

Kwa upande wa wanawake wa kijiji hicho wamedai kuachiwa majukumu ya kifamilia na waume zao hali inayopelekea kutaka kujishughulisha na biashara ndogo ndogo ili kulea watoto wao.

“Mwanaume anaweza kutoka akirudi anadai chakula, tena anaweza kukupiga wakati hajaacha hata pesa ya chakula wala mboga, hivyo ili kuhakikisha familia inakula inakubidi wewe mwanamke uhangaike,” amesema mmoja wa wanakijiji.

Hata hivyo, mshauri wa masuala ya kijinsia, vijana na makundi maalum kutoka shirika hilo, Magdalena Thomas amesema wamebaini wananchi wa kijiji hicho hawana uelewa wa kutosha wa masuala ya ukatili wa kijinsia pamoja na afya ya uzazi, hivyo shirika linaendelea kufanyia kazi jambo hilo, pamoja na kuhamasisha wadau wengine kufika kutoa elimu hiyo.

Chanzo: Uhuru

Send this to a friend