
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya limesema limeanza uchunguzi wa kuwabaini watu watano wasiojulikana ambao wanatuhumiwa kuwakamata watu watatu wakazi wa Kijiji cha Itiryo Wilaya ya Kipolisi Nyamwaga.
Watu waliokamatwa na watu hao wanatambuliwa kama Muriba Muhere (41), Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kata ya Itiryo, Lucas Chacha maarufu kama Kamanda (71) pamoja na Mwita Gesabo (45) wote wakazi wa Kijiji cha Itiryo.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Jeshi la Polisi, imesema Februari 09, 2025 majira ya saa saba usiku katika kijiji hicho, watu watano wakiwa na silaha za moto waliruka ukuta wa nyumba ya Muriba Muhere kisha kumkamata. Baada ya tukio hilo walifika kwenye makazi ya Lucas Chacha na Mwita Gesabo kisha kuwakamata na kuondoka nao.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye taarifa inayoweza kusaidia uchunguzi kufika mahali husika.