Daktari bingwa wa magonjwa ya Ngozi kutoka Hospitali ya Lugalo, Dkt. Msafiri Kombo amesema kitendo cha wanawake kuchangia nywele bandia kina madhara kiafya.
Daktari amesema kuchangia nywele bandia kunaweza kusababisha magonjwa ya ngozi na kuambukizana ikiwamo mba, fangasi na wadudu kama chawa.
“Hatari ya kuvaa wigi lililovaliwa na mtu mwingine ipo sehemu mbili, hapo mtu anaweza kupata maambukizi ya fangasi au wadudu wanaopenda kukaa kwenye nywele ikiwamo chawa kama litakuwa halijasafishwa na vifaa vinavyoangamiza vimelea vyake,” amesema.
Aidha, ameshauri wanawake kuacha kuvaa vitu vilivyovaliwa na watu wengine kama vile nguo na mawigi ili kujiepusha na magonjwa ya ngozi yanayo ambukizwa.
“Kikubwa wajitahidi wanunue yao wenyewe, kuazima nguo, viatu na mawigi haishauriwi kiafya, ni muhimu kila mmoja hasa wanawake kuwa makini na vitu kama hivyo kwa sababu wanapoambukizwa wao ni rahisi kuambukiza watu walio ndani ya familia hususani watoto ambao wanakuwa nao kwa ukaribu,” ameongeza.