Wanawake wawili washikiliwa kwa unyang’anyi wa pikipiki

0
79

Jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro linawashikilia wanawake wawili kwa tuhuma za unyang’anyi wa pikipiki na fedha kwa kutumia silaha aina ya nondo pamoja na panga.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeeleza kuwa wanawake hao waliojulikana kwa majina ya Farida Charles (26) Mkulima na mkazi wa mtaa wa Uchagani Gairo na Grace Chiduo (24) Mkulima mkazi wa kitongoji cha Sambweti Gairo walitekeleza tukio hilo Agosti 13, 2024 baada ya kumkodi mwendesha pikipiki ya abiria (bodaboda), Ndoni John (32) Mkazi wa kitongoji Kichangani Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara akiwa kijiweni kwake na kumtaka awapeleke Sambweti Gairo.

Baada ya kufanikiwa kumkodi dereva bodaboda, walimvamia njiani kwa ushirikiano na wenzao wanaume wawili waliotokea vichakani na kumshambulia kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumnyang’anya pikipiki na pesa taslim Shilingi 4000.

“Baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo Jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo kwa kwa kushirikiana na Kiteto lilifanya msako mkali wa watuhumiwa hao na kuwakamata waanawake hao wakiwa na pikipiki hiyo pamoja na fedha,” imeeleza taarifa.

Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa hao katika kituo cha Polisi Gairo kwa mahojiano na watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Send this to a friend