Wanawake wawili wauawa Geita, mmoja akatwa sehemu za siri

0
54

Watu wawili ambao wote ni wanawake waliotambulika kwa majina ya Bigile Mweshemi (53) Mkazi wa Kijiji cha Nyabulanda na Melesiana Shija (70) mkazi wa Kijiji cha Nyugwa wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wameuawa kwa kukatwa na mapanga huku mmoja akikutwa ameondolewa sehemu za siri.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamhuri Wiliamu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema tukio la kwanza limetokea Kijiji cha Nyabulanda alfajiri ya Januari 16 wakati mama huyo akiwa shambani kwake.

Jamhuri amesema aliyeuawa na kukatwa sehemu za siri ni Bigile Mweshemi huku chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kuwa ni mgogoro wa kifamilia pamoja na imani za kishirikina.

“Aliondoka kwenda shambani alfajiri kwa hiyo hao wakataji mapanga walimvamia na kumkata na mbaya zaidi wakaondoka na sehemu za siri mambo mengine yanatisha ndugu zetu hawa wana mambo magumu sana.

Mmoja anayeshukiwa ambaye ni ndugu wa karibu wa aliyekuwa na mgogoro wa shamba kwa sasa ametoweka na wanaendelea kumsaka huyu ndiye anaedaiwa kuwatuma wakata mapanga,” amesema Jamhuri.

Amesema tukio jingine limehusisha kikongwe aliyetambulika kwa jina la Melesiana Shija aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na wauaji kutokomea kusikojulikana.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio hayo na hadi sasa watu watatu wanashikiliwa na jeshi hilo.

Send this to a friend