Wanne mbaroni kwa tuhuma za unyang’anyi wakiwa na jeneza Mabwepande

0
45

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wanne wanaoendelea kuhojiwa kwa tuhuma za kufanya vitendo vya unyang’anyi, uporaji na kujeruhi wananchi katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imesema tukio hilo limetokea Januari 8, 2026 saa 8:40 mchana katika eneo la Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, karibu na kituo cha Mwendokasi.

Kamanda Muliro amesema kundi la watu ambao wengi wao wakiwa wamepanda pikipiki na baadhi wakiwa na mapanga, walifanya vitendo vya unyang’anyi na uporaji huku wakiwa wamebeba jeneza la marehemu Ibrahimu Elia, mkazi wa Mabwepande.

Ameeleza kuwa marehemu Elia anadaiwa kuuawa Januari 2, 2026 katika eneo la Bunju, baada ya kushambuliwa na kundi la wananchi waliomtuhumu kujihusisha na uporaji wa pikipiki maeneo ya Goba. Hata hivyo ndugu halisi wa marehemu wamefanikiwa kumzika katika makaburi ya Mabwepande.

Katika tukio hilo, watu wanne wameripotiwa kuporwa mali zao huku wengine wakijeruhiwa. Miongoni mwa waathirika ni Japhet Kalanga (41), mfanyabiashara mkazi wa Mabwepande, ambaye amejeruhiwa kichwani na kuporwa simu yake.

Mwathirika mwingine ni Joshua Leguna (26), mkazi wa Mabwepande, ambaye amejeruhiwa puani na mkono wa kulia, na kuporwa simu pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi 20,000.

Send this to a friend