Wanne wafikishwa mahakamani kwa kuteka na kumlawiti mwanablogu Mombasa

0
66

Watu wanne wamefikishwa katika mahakama ya Shanzu kaunti ya Mombasa nchini Kenya na kushtakiwa kwa utekaji nyara na kumlawiti mwanablogu mnamo Septemba 12, 2024.

Mwanablogu huyo amedai kuwa kundi la watu 20 walimteka nyara nyumbani kwake Bamburi, kumpiga na kulawiti eneo la Miritini kabla ya kumtupa karibu na eneo la taka la Mwakirunge.

Ameongeza kuwa waliomshambulia walivamia nyumba yake na kumtaka aandamane nao mahali pasipojulikana ili kuomba msamaha kwa kukosoa serikali ya Kaunti ya Mombasa, na kudai kuwa wangemrudisha nyumbani lakini haikuwa hivyo, kwani alipelekwa hotelini na kuingizwa kwenye gari binafsi huku mikono na miguu yake ikiwa imefungwa.

Kisha mwathiriwa anadai kuwa alifungwa kwenye gunia na kupelekwa eneo la Miritini ambako anadai alivamiwa na kulawitiwa na watu wawili wasiojulikana, baada ya kuhojiwa kuwa ni kwa nini alikuwa akiishambulia serikali ya Kaunti ya Mombasa.

Mwathirika huyo ameeleza kuwa baada ya kitendo hicho alitelekezwa akiwa kwenye gunia na kuokolewa na msamaria mwema ambaye alimsaidia na kuripoti kituo cha polisi cha Bamburi ambapo kufikia Septemba 21, polisi waliwakamata washukiwa watatu wanaoaminika kuwa sehemu ya kundi la watu waliopanga na kulawiti mwanablogu huyo mwenye umri wa miaka 25.

Kulingana na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika kaunti hiyo James Lelia, mmoja wa washukiwa hao alikuwa mwanaume anayedaiwa kutekeleza unyanyasaji huo, huku wengine wawili wakiwa ni wanawake wanaoaminika kupanga uhalifu huo. Hata hivyo washitakiwa wote wamekana mashitaka.

Send this to a friend