Wanne wakamatwa kwa kurusha fedha sakafuni kwenye sherehe

0
66

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuharibu noti za benki kwa kuzirusha sakafuni kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo imesema, Julai 18, 2024 zilisambaa picha za video zikionesha watu wakiwa kwenye sherehe wakiwa wanatoa zawadi za fedha za noti kadhaa za TZS elfu kumi na dola za Kimarekani kwa kuzirusha sakafuni huku watu wengine wakizoa fedha hizo na kuziweka kwenye kapu la zawadi.

“Baada ya kufanya uchunguzi ilibainika kwamba tukio hilo lilifanyika Julai 06, 2024 usiku katika Hoteli ya Kwatunza beach ambapo kulikuwa na hatusi ya Robert Shija ambapo katika harusi hiyo baadhi ya wageni waalikwa walihusika katika utoaji wa zawadi kwa kuzirusha sakafuni kisha fedha hizo kuzolewa na kuwekwa kwenye kikapu,” imeeleza taarifa.

Imeongeza kuwa “Kitendo hicho kilionesha taswira mbaya katika suala zima la utunzaji wa fedha za Kitanzania ambazo ni tuna ya taifa letu.”

Aidha, watuhumiwa hao waliohusika katika tukio hilo wametajwa kuwa ni Majani Masagati (47), Kiruma Lucas (31), Sharifu Juma (29) na Selemani Mbuga (39) na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Jeshi la Polisi limetoa rai kwa Watanzania kuzingatia utunzaji sahihi wa fedha kwani viitendo vya kuchafua fedha kwa makusudi, kuzikanyaga, kuzichora, kuzichana, kuzikusanya na kuzihifadhi kama uchafu na kuzikunja vinafifisha uhai wa fedha hizo.

Send this to a friend