Jeshi la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kurekodi na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu gari aina ya Toyota Noah inayotumika kuwateka watoto katika maeneo mbalimbali.
Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kwamba watoto wawili wanaosoma Shule ya Msingi Vigwaza wametekwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo amesema watu wao ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwa Zoka, Shomari Zinga, (64) Aishi Ally (32), Alphonce Temba (34) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vigwaza na Paul Mwanilezi.
“Taarifa hizi zilienea kwa haraka hadi Shule ya Msingi Mtongani iliyopo Mlandizi wilayani Kibaha na kuleta taharuki kwa wazazi, walimu na Watoto wa shule hiyo ambapo mzazi Zaituni Shabani alieleza kuwa mtoto wake Isimaiya Zuberi (6) ni miongoni mwa watoto waliotekwa,” ameeleza.