Wapona Selimundu baada ya kupandikiza Uloto Hospitali ya Benjamini Mkapa

0
59

Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma imeandika historia ya watoto watatu kupona ugonjwa wa Sikoseli baada ya kuwafanyia matibabu ya upandikizaji wa Uloto.

Akitoa taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Alphonce Chandika amesema baada ya matibabu watoto hao hawana tena maradhi ya Selimundu, na kwamba serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu imewekeza zaidi ya bilioni 3.6 kuwezesha huduma hizo ili kuokoa maisha watanzania.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1 katika bajeti ya Mwaka huu wa Fedha kwa ajili ya Matibabu ya Selimundu, hakuna hata mzazi mmoja ametoa fedha, gharama zote zimebebwa na serikali,” amesema Dkt. Chandika.

Akitoa ushuhuda mmoja wa watoto waliopona ugonjwa huo, Elisha John (11), kwa niaba ya watoto wenzake amesema changamoto zote alizokuwa akizipitia kutokana na sikoseli zimetoweka baada ya matibabu.

“Nilikuwa napata shida ya kuumwa kichwa, damu yangu ilikuwa haizidi sita, shuleni nilikuwa simalizi mwezi, lazima nitalazwa wiki nzima, sihudhurii vipindi shule, tangu nimetibiwa sijasikia maumivu yoyote, ”ameeleza mtoto Elisha.

Send this to a friend