Waraka wa Kinana na Makamba ni utoto- Rais Mstaafu, Mzee Mwinyi

0
37

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi ameelezea kutofurahishwa kwake na kitendo kilichofanywa na aliyekuwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba kutumia picha yake katika mitandao ya kijamii muda mfupi baada uteuzi wake kutenguliwa na Rais Magufuli.

Mzee Mwinyi amesema picha iliyotumiwa na January Makamba katika mitandao ya kijamii ikimuonesha yeye ameketi na January Makamba wakicheka muda mfupi baada ya kufukuzwa Uwaziri imemkwaza kutokana kutumiwa katika mazingira na wakati usiostahili.

Mzee Mwinyi anasema picha hiyo ilipigwa zamani wakati January Makamba alimpomtembea kwa ajili ya kupata uzoefu wake kwa kuwa nae aliwahi kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira na pia alikwenda kumuomba aandike dibaji katika kitabu chake.

Kuhusu waraka ulioandikwa na Makatibu Wakuu Wastaafu Ndg. Abdulrahman Kinana na Ndg. Yusuf Makamba kwenda kwa Baraza la Viongozi Wastaafu, Mzee Mwinyi amesema huo ni Utoto.

Mzee Mwinyi amepongeza majibu yalitolewa na Katibu wa Baraza hilo Mzee Pius Msekwa na kusema walioandika waraka huo wameshindwa kufuata katiba na taratibu za chama na kwamba viongozi wastaafu hawawezi kupoteza muda wao kwa masuala ya kitoto.

Mzee Mwinyi amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya kuleta maendeleo kwa muda mfupi.

Amebainisha kuwa ukiondoa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere viongozi wengine waliofuata akiwemo yeye wamefanya juhudi za kuipeleka nchi mbele lakini kasi ya Rais Magufuli ni kubwa zaidi.

Mzee Mwinyi amezungumza hayo nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam, leo Julai 22, 2019.

Send this to a friend