Wasafiri kutoka nje ya nchi kupelekwa karantini Hosteli za Magufuli

0
39

Na WAMJW-Dar es Salaam

Serikali imetangaza rasmi kwamba wasafiri wote kutoka nchi za nje zilizoathirika na ugonjwa wa Corona watalazimika kukaa karantini kwa muda wa siku 14 katika hosteli za Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam maarufu hosteli za Magufuli.

Akizungumza katika hosteli za Magufuli, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wasafiri hao watafikia katika hosteli za Magufuli ambazo zipo katika eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam.

“Lengo ni kuhakikisha tunadhibiti mienendo ya wasafiri hawa.Tumeona taarifa ambazo zimetoka kule Iringa, kuna baadhi ya wasafiri tuliwaweka hotelini wakatoroka sasa ili kudhibiti mienendo ya wasafiri hawa na kuwalinda Watanzania wengi tumeona kuna ulazima wa kuwaweka sehemu moja ambako kutakuwa na ulinzi wa saa 24 na mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Dar es Salaam,Bw. Paul Makonda atasimamia kwa karibu chini ya Wizara ya Afya,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy Mwalimu amewataka wananchi waelewe kwamba wasafiri hao si wagonjwa kwa sababu wanatoka kwenye nchi zenye maambukizi yenye virusi vya Corona (Covid-19) hivyo wasichukuliwe kama ni wagonjwa.

“Tunawachukulia kwamba miongoni mwao kuna mmoja, wawili au watu watatu wakawa na maambukizi ya virusi vya Corona.

Tutawaweka hapa kwa siku 14 kwa lengo la kuwaangalia afya zao, itakapofika siku 14, wale ambao hawajaonyesha DALILI zozote tutawaruhusu waende majumbani kwao lakini wale watakaoonyesha dalili ndani ya siku tano, sita, Saba, nane hadi siku ya 14 tutachukua sampuli na kuwapima ili kujiridhisha Kama wana virusi vya Covid-19,” amesema Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy Mwalimu amesisitiza kuwa kwa mujibu wa taarifa za maambara Hali ya wagonjwa waliopata maambukizi ya Covid-19.“Tuko vizuri, watu waliopata maambukizi ni 20, tumepata kifo kimoja, wagonjwa watatu wamepona na wamesharudi nyumbani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameishukuru Wizara ya Afya kwa namna ambavyo Imekuwa ikipambana kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Corona nchini.

“ Sisi Kama Mkoa tumejipanga kuhakikisha kwamba watu wote wanaokuja na ambao wapo wanakuwa na afya Njema kwa ajili ya kujenga uchumi wa Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla.

“Maelekezo ambayo ameyatoa mheshimiwa waziri wa Afya ni maelekezo ambayo kila anayeingia kwenye Mkoa huu kutoka nchi yoyote, Magufuli hoteli inamuhusu,” amesema Paul Makonda.

Makonda amewataka Watanzania kufanya kazi na kwamba kuanzia kesho jumatatu atawakamata wazururaji wote wanaozunguka mjini bila kuwa na kazi maalumu watakamatwa kwa kuwa wanasababisha mikusanyiko isiyokuwa na tija.

Mwisho.

Send this to a friend