Tasnia ya muziki nchini Tanzania inazidi kukua kila siku kufikia kiwango cha kuwawezesha wasanii kuendesha maisha yao na kufanya uwekezaji mkubwa jambo ambalo kwa miaka kadhaa kipindi cha nyuma lilikuwa ni changamoto.
Kupitia mitandao ya kijamii, hasa YouTube, wasanii wanaweza kuingiza vipato ambavyo vinatokana na idadi ya watu waliotazama nyimbo zao. Hii ikiwa na maana kwamba, kadiri nyimbo zako zinavyotazamwa zaidi, unakuwa kwenye nafasi ya kuingiza fedha nyingi zaidi.
Hapa chini ni orodha ya wasanii watano wa Tanzania waliotazamwa zaidi (ndani ya Tanzania) kupitia mtandao wa YouTube kwa mwaka mmoja uliopita kuanzia Mei 1, 2019 hadi Mei 1, 2020
Mwanamuziki Diamond Platnumz ameendelea kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania, ambapo kwa mujibu wa Billboard, mwanamuziki huyo ndiye aliyeongoza kwa kutazamwa mara nyingi zaidi nchini Tanzania.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka mmoja uliopita, msanii huyo anayetamba na nyimbo kadhaa kama vile Baba Lao na Jeje ametazamwa mara milioni 53.94.
Nafasi ya pili inashikwa na Harmonize ambaye ametazamwa mara milioni 39.66, huku mtoto wa Mbeya, Rayvanny akishika nafasi ya tatu kwa kutazamwa mara milioni 30.21.
Itakumbukwa wasanii hao wawili (Harmonize na Rayvanny) wamekuwa chini ya usimamizi wa lebo ya WCB ambayo inamilikiwa na Diamond Platnumz (Rayvanny bado yupo WCB).
Nafasi ya nne inashikwa na mfalme wa bongo fleva, King Alikiba ambaye yeye ametazamwa mara milioni 14.15, huku nafasi ya tano ikienda kwa Aslay aliyetazamwa mara milioni 13.73.
Ikumbukwe takwimu hizi ni za ndani ya Tanzania, hazihusishi idadi ya watu waliotazama wasanii hawa kutoka nje ya Tanzania (global views).
Aidha, Billboard imetoa takwimu nyingine kuhusu muziki na wasanii kutoka barani Afrika, ambapo katika takwimu hizo, Diamond Platnumz ameshika nafasi ya 14 kati ya wasanii 15 waliotazamwa zaidi barani Afrika.
Pia, ameshika nafasi ya pili kati ya wasanii 15 waliotazamwa zaidi Kusini mwa Jangwa la Sahara. Katika orodha hii, Harmonize ameshika nafasi ya tisa, huku Rayvanny akiwa wa 10.