Wasanii wanaohamasisha uvutaji bangi kuwajibishwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya amewaonya wasanii wa Tanzania wanaotunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na kusema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wasanii hao.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Desemba 7, 2022 jijini Dar es salaam Kusaya ameeleza kuwa hatua zitachukuliwa kwa wasaniii ambao hawatumii kipaji chao kuwaelimisha watu badala yake wanatunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya.
“Kama kuna msanii anadhani anaweza kupata umaarufu kwa kupitia nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya hatutomuacha hata mara moja, sheria itachukua mkondo na ipo siku nitawaita waandishi wa habari ili muone kitu gani tumekifanya kwa wasanii wanaotaka kupata umaarufu kwa kutumia dawa za kulevya.
Mbona mashairi yapo ya aina nyingi unashindwaje kutunga mashairi ya vitu vyote, si wahamasishe hata kilimo bora au biashara, kwani lazima wahamasishe mambo ya bangi? hatutoruhusu Mtanzania yoyote afanye uhamasishaji wa matumizi ya dawa za kulevya” amesema Kusaya.