Wasifu mfupi wa Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania

0
18

DAR ES SALAAM – Katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dk. John Pombe Magufuli jana alipokea hati za utambulisho za Balozi Mpya wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Donald J. Wright. Dr. Wright anakuwa Balozi wa 19 wa Marekani nchini Tanzania.

Balozi Wright alimhakikishia Rais Magufuli uimara wa ushirikiano wa Marekani na Tanzania, akisema “Natarajia kufanya kazi ya kuimarisha uhusiano wetu wa nchi mbili katika Nyanja za afya, usalama, utawala, na elimu.”

Balozi Donald J. Wright aliapishwa kama Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 2 Aprili 2020 jijini Washington, D.C. Kwa miaka 17 iliyopita Balozi Wright amekuwa kiongozi katika afya ya umma na sera za afya katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Hii ni pamoja na kuhudumu katika Wizara ya Afya na Huduma za Binadamu ya Marekani, Wizara ya Kazi na Ajira na Umoja wa Mataifa.

Kabla ya uteuzi wake kama Balozi nchini Tanzania, Balozi Wright alikuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Huduma za Binadamu (Department of Health and Human Services – HHS), hiki ni chombo cha juu kabisa nchini Marekani kinachohusika na masuala ya afya.

Hali kadhalika, aliongoza Idara ya Kudhibiti Maradhi na Kukuza Afya (Office of Disease Prevention and Health Promotion – ODPHP), Ofisi ya Kusimamia Uadilifu katika Tafiti (Office of Research Integrity – ORI) na Idara ya Usalama wa Afya Kazini (OSHA). Pia alihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Rais la Michezo, Utimamu wa Kiafya na Lishe (President’s Council on Sports, Fitness and Nutrition – PCSFN.)

Kwa takribani miongo miwili kabla ya kuingia katika utumishi serikalini, Dk. Wright alikuwa daktari akihudumu katika jimbo alilotokea la Texas, akibobea zaidi katika afya ya familia na usalama wa afya kazini.

Anaungana nchini Tanzania na mkewe Kathy.

Send this to a friend