Wasifu mfupi wa CAG mpya, Charles Kichere

0
57

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemteua Charles Kichere kuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwa mujibu wa taarifa nchini, CAG huyo mpya Kichere anatarajiwa kuapishwa rasmi leo Jumatatu asubuhi.

Kichere anaichukua nafasi ya Profesa Assad Mussa, mkaguzi anayeondoka kufuatia kumalizika kwa muda wake wa uhudumu tarehe 4 Novemba.

Kabla ya wadhifa huu mpya, Kichere alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe nchini.

Charles Kichere ni nani?

Alisoma elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na Chuo Kikuu cha Tumaini, jijini Dar Es Salaam.

Kichere aliwahi kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mnamo tarehe 25 Machi mwaka 2017, aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Kamishna Mkuu wa TRA. Aliipokea nafasi hiyo kutoka kwa Alphayo Kidata ambaye aliteuliwa wakati huo kuwa Katibu Mkuu Ikulu Tanzania.

Charles Kichere alihudumu kama Kamishna Mkuu wa TRA kuanzia Machi 2017 hadi Juni mwaka huu 2019, wakati aliondoshwa katika mamlaka hiyo, katika mabadiliko ya Rais Magufuli aliyotoa Ikulu jijini Dar es Salaam kupitia taarifa rasmi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais.

Kichere aliteuliwa badala yake kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Yuko kwenye bodi ya Benki ya CRDB Tanzania.

Amewahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mweka Hazina na pia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu katika kampuni ya majani ya chai ya Unilever nchini Kenya na Tanzania.

Amepokea wadhifa wa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kutoka wa Profesa Mussa Assad.

Hapa chini ni orodha ya wadhibiti na wakaguzi wa hesabu za serikali Tanzania tangu mwaka 1961:

  1. R.W.A. McColl aliyehudumu 1961 hadi 1963
  2. Gordon. A. Hutchinson aliyehudumu 1964 hadi 1969
  3. Mohamed Aboud aliyehudumu 1969 hadi 1996
  4. Thomas Kiama aliyehudumu 1996 hadi 2005
  5. Ludovick S. L. Utouh aliyehudumu 2006 hadi 2014
  6. Prof. Mussa Juma Assad aliyehudumu 2014 hadi 2019
  7. Charles Kichere, anayehudumu kuanzia leo

HT: bbcswahili

Send this to a friend