Wasifu mfupi wa Mwendazake Mhandisi Mfugale

0
42

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale afariki dunia leo Juni 29, 2021.

Mfugale ambaye ni mbobezi katika sekta ya ujenzi aliteuliwa kushika wadhifa huo Mei 2011.

Katika miaka 10 ya kuiongoza TANROADS atakumbukwa kwa mengi lakini zaidi ni uhodari wake katika ujenzi wa madaraja. Alifanikiwa kujenga madaraja yaliyoweka alama nchini ambayo ni pamoja na Daraja la Mkapa kwenye mto Rufiji, Daraja la Rusumo katika Mto Kagera, Daraja la Kikwete, kwenye mto Malagarasi, Daraja la Nyerere, Kigamboni, Daraja la Mfugale na Daraja la Kijazi mkoani Dar es Salaam.

Daraja la Juu la Mfugale lililopo katika makutano ya barabara za Nelson Mandela na Nyerere lilipewa jina lake kama alivyoeleza Hayati Dkt. John Magufuli wakati wa uzinduzi kuwa ni kutokana na utendaji kazi wake ulioimarq, na sio upendeleo.

Kabla ya uteuzi huo, Mfugale alikuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS na aliwahi kushika nafasi mbalimbali katika serikali na kusimamia ujenzi wa barabara na madaraja muhimu kwa taifa.

Aidha, Mfugale pia aliwahi kushika majukumu maalumu katika wizara ya ujenzi kama Mkurugenzi wa Idara ya Barabara za Mikoa.

Mfugale alizaliwa katika eneo la Ifunda, mkoa wa Iringa na kumaliza elimu ya upili katika shule ya Moshi mwaka 1975.

Alikuwa na Shahada ya Uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Roorkee India, na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu Loughborough cha Uingereza, ni mhandisi alisajiliwa na alihudhuria mafunzo ya Ujenzi na uchumi, Mafunzo ya miradi na utunzaji wa barabara pamoja na ujenzi na utunzaji wa madaraja.

Mwaka 2003 alipewa tuzo na Bodi ya Wahandisi wa Tanzania na mwaka 2018 alitunukiwa tuzo nyingine iitwayo “Engineering Execellency,” yote ikiwa ni kutambua mchango wake katika sekta ya ujenzi.

Aidha, Patrick Mgufale alitengeneza mfumo wa usimamizi madaraja uitwao “Bridge Management System.”

Send this to a friend