Wasifu mfupi wa Profesa Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili

0
136

Profesa Mohamed Janabi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliyebobea kwenye magonjwa ya moyo. Amekuwa akishauri masuala ya ulaji unaozingatia afya ili kuepukana na magonjwa mbalimbali na kuishi bora.

Kupitia uzoefu wake wa kitabibu na taaluma yake, Profesa Janabi ametoa mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii, ambapo mbali na kuwa mkurugenzi wa hospitali, amejitolea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa lishe bora na mtindo wa maisha wenye afya.

Profesa Janabi amekuwa na safari ndefu ya kitabibu akianza mafunzo yake ya tiba nchini Ukraine, ambapo alikaa kwa kipindi cha miaka sita kabla ya kwenda Uingereza kwa ajili ya kupata mafunzo ya kliniki kwa wahitimu (Junior housemanship) ambapo alikaa kwa mwaka mmoja.

Baada ya hapo alirejea Tanzania ambapo alijitolea mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadaye alifanya kazi kabla ya kwenda kusomea Shahada ya Uzamili nchini Australia kwa miaka mitatu, na kisha kuajiriwa nchini Ufilipino ambapo alifanya kazi mwaka mmoja na Red Cross Internal kisha kurejea nchini.

Alipata ufadhili wa masomo nchini Japan kwa ajili ya kujiunga na Shahada ya Uzamivu (PhD) kuhusu magonjwa ya moyo ambapo ilimchukua miaka mitano kabla ya kuhitimu masomo yake na kisha kupata ‘fellowship’ na kuhamia Marekani na kujiunga na Medical University of South Carolina (MUSC).

Baada ya kurejea nchini Tanzania, mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Daktari wa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye mpaka sasa bado anahudumu nafasi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano kuhusu kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anasema “tulikuwa kwenye ziara ya China 2010/11 hivi, na Mheshimiwa Rais alituuliza sisi wasaidizi wake; leo nina mkutano na mwenyekiti wa China, nini ambacho cha ziada tunacho, ndipo lilipokuja wazo la Jakaya Kikwete.”

Miaka 22 kati ya umri wake alio nao sasa ameutumia katika elimu ngazi ya chuo kikuu na sasa anatarajia kupokea shahada ya Geriatrics Medine (matibabu watu wazima) ambapo alijiunga na chuo cha Cardiff cha Uingereza miaka miwili iliyopita.