Wasifu wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Hayati Job Ndugai

0
177

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai amefariki dunia Agosti 06, 2025 hospitalini wakati akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, Marehemu alifariki dunia kutokana na shinikizo la damu kushuka sana (sceptic shock) iliyosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa (severe pneumonia).

Taarifa za kifo chake zimetangazwa na Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson.

Job Yustino Ndugai alikuwa mwanasiasa kutoka Tanzania ambaye alihudumu kama Spika wa Bunge tangu mwaka 2015. Kabla ya hapo alihudumu kama Naibu Spika wa Bunge tangu mwaka 2010.

Wasifu wa Hayati Job Ndugai

Alizaliwa Januari 21, 1963 alipata elimu ya msingi kutoka Shule ya Msingi Mtare kuanzia mwaka 1991-1997. Alianza elimu ya Sekondari ya Kibaha mwaka 1978-1981 na kumalizia Shule ya Sekondari Old Moshi kuanzia 1982-1984.

Alisoma Stashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori kutoka Chuo cha Mweka kuanzia mwaka 1986-1988, kisha Shahada ya Kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1989-1993).

Alisoma Post Graduate kutoka Chuo cha Kilimo nchini Norway kuanzia 1994-1995 na kusoma Shahada ya Umahiri kutoka chuo hicho (1995-1996).

Safari yake ya elimu iliishia Eastern and Southern African Management Institute ambapo alisoma Shahada ya Umahiri katika Usimamizi wa Biashara (2005-2008).

Mafanikio ya kitaaluma na tuzo

Wakati wa safari yake kimasomo Marehemu Ndugai alipata tuzo zifuatazo za kitaaluma.

1. Mwaka 1988 alipata tuzo ya Mwanafunzi Bora wa jumla katika Chuo cha Wanyamapori Mweka.

2. Mwaka 1993 alipata tuzo ya Mwanafunzi Bora (Outstanding Best Student) katika Kitivo cha Zolojia na Botania Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

3. Mwaka 1996 alipata tuzo ya Mwanafunzi Bora (Best Student) Katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Norway (AUN).

Kazi na Ajira

Marehemu Ndugai aliajiriwa katika Utumishi wa Umma na kushika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo:-

• Mwaka 1988 – 1989: Afisa Msaidizi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

• Mwaka 1993–1994: Meneja Mradi wa Ukanda wa Mashariki wa Hifadhi ya Selous.

• Mwaka 1997–2000: Aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mradi wa Uhifadhi wa Kanda ya Serengeti, uliohusisha jamii za jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kanda ya Uhifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi za Maswa, Ikorongo na Grumeti.

Safari ya kisiasa

• Marehemu alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mwaka 2000 na ameendelea kuwa Mbunge wa Jimbo hilo hadi 3 Agosti, 2025.

• Mwaka 2001 – 2005: Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Mazingira.

• Mwaka 2005 – 2010: Mwenyekiti wa Bunge na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Mazingira.

• Mwaka 2006 – 2007: Marehemu Ndugai aliongoza Kamati Maalumu ya kufanya marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo ilileta mageuzi makubwa kwenye uendeshaji wa Bunge.

• Mwaka 2010 – 2015: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

• Mwaka 2015 – 2022: Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alichaguliwa kuwa spika baada ya kupata kura 254 kati ya 365, na mpinzani wake Goodluck Ole Medeye kutoka CHADEMA akipata kura 109, huku kura mbili zikiharibika.

Moja ya mambo yatakayo kumbukwa akiwa katika uongozi wake wa bunge, ni pamoja na mijadala kadhaa ikiwemo sakata la wabunge 19 wa CHADEMA waliokuwa wamevuliwa uanachama wao, na kuhojiwa kwa baadhi ya wabunge akiwemo Josephat Gwajima na Jerry Muro kwa madai ya kushusha hadhi na heshima ya bunge.

Januari 6, 2022 alijiuzulu nafasi ya Uspika kutokana na sababu binafsi na kwa hiari yake.

Hayati Job Ndugai alikuwa akiwania kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo Kongwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Send this to a friend