Wasifu wa Brigedia Jenerali Ezra Ndimgwango aliyefariki

0
29

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo ametangaza kifo cha Afisa Mkuu Brigedia Jenerali, Ezra Wilson Ndimgwango (Mstaafu), kilichotokea Februari 3, 2021 katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo.

Marehemu alizaliwa Desemba 30, 1953 katika Kijiji cha Shunga, Kata ya Shunga, Tarafa ya Buhoro, Wilaya ya Kasulu katika Mkoa wa Kigoma.

Alipata elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Project Management mwaka 2000 hadi 2001 nchini Tanzania na Conflict Management nchini Zimbabwe mwaka 2001.

Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Mei 2, 1974. Alihudhuria kozi mbalimbali ikiwemo kozi ya Afisa Mwanafunzi nchini Canada na kutunukiwa Kamisheni tarehe Juni 1, 1977.

Alipandishwa vyeo ngazi kwa ngazi hadi cheo cha Brigedia Jenerali mnamo Septemba 17, 2012. Alilitumikia jeshi kwa muda wa miaka 41 na miezi 9 hadi alipostaafu utumishi jeshini kwa umri Januari 31, 2016.

Brigedia Jenerali Ndimgwango alitunukiwa medali mbalimbali wakati wa utumishi wake ifuatavyo:- Medali ya vita; Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi Mrefu; Miaka 40 ya JWTZ; Utumishi Uliotukuka; Miaka 50 ya JWTZ; Miaka 50 ya Muungano; Miaka 50 ya Uhuru na Nishani ya Comoro.

Katika utumishi wake jeshini, aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwemo Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Jeshi la Anga mwaka 2009 hadi mwaka 2010 na Mkuu wa Kambi Kikosi cha Usafirishaji wa Anga mwaka 2012, madaraka aliyohudumu hadi anastaafu Jeshi kwa umri Januari 31, 2016.

Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Februari 6, 2021 kuanzia saa 03:00 asubuhi, na mazishi yatafanyika siku hiyo hiyo katika Makaburi ya ‘Air wing’ yaliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam.

Marehemu ameacha mke na watoto.