Wasifu wa David McAllister, mwanasheria na mwanasiasa wa Ujerumani anayemtetea Mbowe Bunge la Ulaya

0
50

 

Wengi mtakuwa mmeona picha na video za David McAllister (pichani) ambaye ni Mbunge wa Bunge la Ulaya na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge hilo, akielezea kukerwa kwake na hali ya upinzani nchini Tanzania, mathalani kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

McAllister ni mwanasiasa nchini Ujerumani (sehemu ya umoja wa Ulaya) na amekuwa moja ya wajumbe wa Bunge la Ulaya kwa miaka saba sasa. Yeye na familia yake, kuanzia wazazi wake wana uraia wa nchi mbili ambazo ni Ujerumani na Uingereza. Januari 12 mwaka huu alitimiza umri wa miaka 50. Nafasi yake ya Uenyekiti katika Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya ameipata mwaka 2017, maana yake amedumu hapo kwa miaka minne sasa.

Aliingia katika siasa za Ujerumani kupitia chama cha Christian Democratic Union (CDU) au Umoja wa Kidemokrasia wa Kikristo, chama cha Waliberali-Wahafidhina wa Mrengo wa Kati. Itikadi ya CDU iko katika misingi mitatu ambayo katiba ya chama hicho inaitaja kuwa ni Demokrasia ya Kikristo (Christian Democracy), Uliberali wa Kihafidhina (Liberal Conservatism) na Maslahi ya Ulaya Kwanza (Pro-Europeanism).

Mjumbe huyu wa Bunge la Ulaya ni mwanasheria kitaaluma. Mbali na kazi yake ya uanasheria na siasa, McAllister ni mwanajeshi mstaafu katika Jeshi la Ujerumani. Amehudumu katika Jeshi hilo kati ya mwaka 1989 hadi mwaka 1991, ikiwa ilikuwa lazima kwa kila Mjerumani kufanya hivyo kisheria. Babaye McAllister, mzee James McAllister naye pia alikuwa mmoja ya wanajeshi muhimu wa Jeshi la Ufalme wa Uingereza (kumbuka familia ina uraia wa Ujerumani na Uingereza) katika kikosi cha ujasusi wa mifumo ya mawasiliano (Royal Corps of Signals).

McAllister si tu mwanasiasa, mwanasheria na mwanajeshi mstaafu lakini pia katika biashara hayuko nyuma na ni muumini wa vitendo wa siasa za ubepari wa kimagharibi. Katika ujana wake alikuwa mmoja ya wanaharakati wa kupinga ujamaa akitetea sera za kibepari za Ujerumani Magharibi. Mwaka 2010 alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya usimamizi wa Kampuni ya Magari ya Volkswagen, kampuni ambayo iko katika jimbo analotokea la Lower Saxony, Kaskazini Magharibi mwa Ujerumani.

Maoni juu ya McAllister yamegawanyika. Nchini Ujerumani ana ufuasi wa wastani kwa watu wa kawaida na wa kutosha katika chama chake cha Umoja wa Kidemokrasia wa Kikristo (CDU). Barani Ulaya amekuwa mpingaji mkubwa wa namna Urusi inavyoendesha mambo yake hasa kwa kusema kuwa nchi hiyo haina demokrasia ya kweli na inavuruga nchi ndogo ndogo majirani zake jambo ambalo Urusi imekuwa ikilipuuza nyakati zote. Mojawapo ya mvutano wake na Urusi ni ule wa Machi 2020 wa kupinga Urusi kuliweka shirika lisilo la kiserikali la European Endowment for Democracy katika orodha ya mashirika yasiyotakiwa Urusi. Katika taarifa yake Urusi ilisema shirika hilo ni hatari kwa usalama na ustawi wa nchi hiyo huku McAllister akiutaka Umoja wa Ulaya kuishinikiza Urusi kuruhusu shirika hilo kuendelea kupokea fedha za wafadhili na kufanya kazi nchini humo.

Sakata jingine ambalo McAllister amevutana na baadhi ya watu ni masuala ya ndani ya migogoro katika nchi kama Belarus, Cameroon, Misri, Tanzania, Ethiopia, na nyinginezo ambapo katika moja ya mahojiano ya televisheni ya Channel 4 News Mei mwaka huu, wachangiaji walimtaka kufuatilia wizi na mapungufu katika Ujerumani na serikali nyingine za Ulaya na kuacha kupoteza muda na kuingilia na masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Kwa upande wa Tanzania, McAllister anamtaka Rais Samia Suluhu kuondoa mashitaka ya ugaidi dhidi ya Mbowe jambo ambalo wachambuzi wa siasa na diplomasia wanasema ni kutaka Rais kuingilia mahakama, kitu ambacho Umoja wa Ulaya inapinga, hivyo ni mkanganyiko. Wachambuzi wanaeleza pia kuwa mbunge huyo hana haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine ikiwemo kushinikiza taasisiza serikali na mahakama kufanya kazi kwa namna ambayo yeye anaona ni sahihi.

Send this to a friend