Wasifu wa maisha ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai

0
48

Job Yustino Ndugai (58) ni mwanasiasa kutoka Tanzania ambaye anahudumu kama Spika wa Bunge tangu mwaka 2015. Kabla ya hapo alihudumu kama Naibu Spika wa Bunge tangu mwaka 2010.

Alizaliwa Januari 21, 1963 alipata elimu ya msingi kutoka Shule ya  Msingi Mtare kuanzia mwaka 1991-1997. Alianza elimu ya Sekondari ya Kibaha mwaka 1978-1981 na kumalizia Shule ya Sekondari Old Moshi kuanzia 1982-1984.

Amesoma Stashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori kutoka Chuo cha Mweka kuanzia mwaka 1986-1988, kisha Shahada ya Kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1989-1993).

Amesoma Post Graduate kutoka Chuo cha Kilimo nchini Norway kuanzia 1994-1995 na kusoma Shahada ya Umahiri kutoka chuo hicho (1995-1996).

Safari yake ya elimu iliishia Eastern and Southern African Management Institute ambapo alisoma Shahada ya Umahiri katika Usimamizi wa Biashara (2005-2008)

Amekuwa mbunge wa Kongwa kwa miaka 21 sasa (tangu mwaka 2000) na ameshika nafasi mbalimbali ndani ya kamati za bunge.

Alichaguliwa kuwa spika wa bunge Novemba 17, 2015 baada ya kupata kura 254 kati ya 365, na mpinzani wake Goodluck Ole Medeye kutoka CHADEMA akipata kura 109, huku kura mbili zikiharibika.

Katika uongozi wake wa bunge, mambo kadhaa yameibua mjadala mkubwa ikiwemo sakata la wabunge 19 wa CHADEMA wanaodaiwa kuvuliwa uanachama wao, na kuhojiwa kwa baadhi ya wabunge akiwemo Josephat Gwajima na Jerry Muro kwa madai ya kushusha hadhi na heshima ya bunge.

Suala jingine ni kumtaka mmoja wa wabunge aliyedai amevaa nguo zisizo za staha kutoka ndani ya ukumbi wa bunge. Uamuzi huo ulikosolewa vikali, wakosoaji wakieleza kwamba vazi la mbunge huyo halikuwa na tatizo. Karibuni, amezua mjadala tena kwa kusema Tanzania haitakiwi kukopa ili kufadhili miradi ya maendeleo.

Mbali na ubunge, amefanya kazi sehemu nyinginezo ikiwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Pori la Akiba Selous na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).

Januari 6, 2022 amejiuzulu nafasi ya Uspika kutokana na sababu binafsi na kwa hiari yake.

Ndugai ni mume wa Fatuma Mganga.

Send this to a friend