Wasifu wa marehemu Balozi Juma Volter Mwapachu

0
7

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu amefariki dunia jana Machi 28, 2025 katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Juma Volter Mwapachu alizaliwa Septemba 27, 1942, huko Mwanza, Tanzania. Alikuwa mwanasiasa mashuhuri wa Tanzania na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya Amanya Mushega wa Uganda kukamilisha muhula wake wa miaka mitano mnamo Machi 24, 2006.

Balozi Mwapachu aliteuliwa kwa nafasi hiyo na Rais wa Tanzania wa wakati huo, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za EAC Aprili 04, 2006. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Elimu na Tuzo za Heshima
Balozi Juma Mwapachu ni mhitimu wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako alipata shahada yake mwaka 1969. Pia ana Stashahada ya Uzamili katika Sheria za Kimataifa, Taasisi za Kimataifa na Diplomasia kutoka Chuo cha Kimataifa cha Sheria na Diplomasia, New Delhi, India.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilimtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu wa Fasihi (Doctor of Literature, Honoris Causa) mnamo mwaka 2005. Aidha, alipata Shahada ya Heshima ya Uzamivu wa Sayansi za Kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Rwanda.

Uzoefu wa Kazi na Uongozi
Mwapachu ni mwanasheria kitaaluma na amepata uzoefu mpana katika sekta mbalimbali, ikiwemo benki, maendeleo vijijini, diplomasia, na sekta binafsi. Miongoni mwa nyadhifa alizowahi kushikilia kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa EAC ni pamoja na:

– Kufanya kazi katika Wizara ya Serikali za Mitaa na Utawala wa Mikoa katika miaka ya 1970.

– Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa kuanzia mwaka 2002 – 2006.

– Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania.

– Mwenyekiti wa bodi za mashirika ya umma, ikiwemo Benki ya Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Bank).

– Kamishna wa Tume ya Rais ya Mageuzi ya Mashirika ya Umma.

– Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (Confederation of Tanzania Industries – CTI) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.

– Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Biashara ya Nje na Baraza la Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

– Mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa (Society for International Development).

– Mjumbe wa Tume mbalimbali za Rais na mmoja wa waandishi wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025.

Balozi Mwapachu amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia majukumu yake mbalimbali katika nyanja za siasa, uchumi, na maendeleo ya jamii.