Wasifu wa marehemu Dkt. Faustine Ndugulile, Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani

0
49

Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile ameaga dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dkt. Ndugulile alikuwa mtaalamu wa afya, mwanasiasa mahiri, na kiongozi wa mfano aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za afya, mawasiliano, na usimamizi wa kimataifa. Alizaliwa tarehe 31 Machi 1969, katika wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Tanzania.

Elimu na Utaalamu

Dkt. Ndugulile alipata elimu ya hali ya juu na kuwa miongoni mwa wataalamu wa kipekee waliochanganya taaluma ya tiba na sheria. Alipata shahada ya Udaktari wa Tiba (MD) mwaka 1997 na Shahada ya Uzamili ya Tiba (MMed) mwaka 2001 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mnamo 2010, alihitimu Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma (MPH) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, Afrika Kusini, na mnamo 2022 alikamilisha Shahada ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Safari ya kisiasa na uongozi

Dkt. Ndugulile alijiunga na siasa mwaka 2010 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Kigamboni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Aliongoza jimbo lake kwa kujituma, akitekeleza miradi ya kuboresha miundombinu, afya, na huduma za kijamii.

Kati ya mwaka 2007 hadi 2010, aliwahi kuwa Mshauri Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini akitoa msaada wa kiutaalam kwa nchi nyingine nyingi kama vile Angola, Msumbiji, Tanzania na Rwanda.

Mnamo Oktoba 2017, Rais wa Tanzania wa wakati huo, Dkt. John Magufuli, alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, akisimamia mipango muhimu ya kuboresha huduma za afya, hususan afya ya mama na mtoto.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akiongoza kwa ubunifu, na kusisitiza matumizi ya teknolojia kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha uchumi wa kidijitali.

Mnamo Agosti 27, 2024, Dkt. Ndugulile alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, nafasi iliyompa heshima kubwa na Tanzania kwa ujumla kwani, ilimuweka mstari wa mbele katika kusimamia na kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika, huku akitarajia kuanza kutumikia wadhifa huo mwezi Februari, 2025.

Pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya ya Bunge la Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa (IPU) Advisory Group Health na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH).

Dkt. Ndugulile ameacha watoto wawili, Martha na Melvin Ndugulile.

Dkt. Faustine Ndugulile atakumbukwa kama kiongozi shupavu aliyewakilisha Tanzania kwa heshima katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa, akiwa mfano wa kuigwa kwa uadilifu na bidii. Mchango wake katika sekta ya afya, mawasiliano, na usimamizi utaendelea kuishi milele.

 

Send this to a friend