Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Arusha (APC) kimeeleza kusikitishwa na kulaani kitendo cha baadhi ya waandishi wa habari kutishiwa kutokana na kuripoti mwenendo wa kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
APC imesema kuwa imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari waliopigiwa simu za vitisho, na watu wasiojulikana, ambao wameonesha kukerwa na namna kesi ya Sabaya na wenzake inavyoripotiwa na waandishi.
Mbali na kupiga simu, watu hao inadaiwa kuwa wamwdiriki kufika nyumbani kwa mmoja wa waandishi wa habari mara tano wakimtafuta lakini mara zote hawakumkuta, na kwamba haijulikani nini kingetokea endapo wangemkuta.
APC imesema kuwa inaamini vyombo vya ulinzi na usalama vitachukulia suala hilo kwa uzito mkubwa na kuhakikisha usalama wa waandishi wakitekeleza majukumu yao.
Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashitaka mbalimbali yakiwemo ya kuunda genge la uhalifu, rushwa, unyang’anyi wa kutumia silaha na utakatishaji fedha haramu.