Wasira: Hakuna uhuru wa kutoa maoni kwa kutukanana mitandaoni

0
4

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira amesema hakuna uhuru au demokrasi ya kutukana mitandaoni na wala hakuna uhuru usio na mipaka.

Akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa Chama hicho wilayani Songea Vijijini mkoani Ruvuma, Wasira amesema kumekuwepo na tabia ambayo si utamaduni wa Watanzania wa kuona ni jambo la kawaida kutukanana katika mitandao ya kijamii.

“Lakini hebu niulize wazee watuambie hivi huku (Songea) katika mila na utamaduni watoto walikuwa wanatukana baba zao, walizuiwa na nani? Walizuiliwa na utamaduni. Watoto hawakuwa na nafasi ya kumtukana baba wala mama, hata kama atakuwa amekosea bali walikuwa wamejiwekea utaratibu tofauti na wa demokrasia ya sasa,” amesema Wasira.

Wasira amefafanua kuwa uhuru ni kutoa maoni kwa kufuata sheria maana unaweka sheria ambazo zinaifanya jamii iishi pamoja bila ya bughudha ili kuondoa mtu asimuonee mwingine, na kwamba kwa mujibu wa sheria za Tanzania kutukana ni kosa la jinai.

“Uhuru wa kutukanana sasa hapo tumekosea njia, ungekuwa uhuru wenyewe ni wa kutukanana tungeutafuta wa nini? Tulitafuta uhuru ili utusaidie kujenga watu pamoja na kuleta amani katika kuleta nchi na kusimamia maendeleo yao.”

Aidha, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, wagombea waache mtindo wa kizamani wa kufikiri kwamba wanaweza kushinda nafasi za uongozi kwa kugawa fedha kwa wajumbe au wapigakura kwakuwa mgombea atashinda kutokana na kazi zake.