Wastani wa kodi kwa Kaya nchini wafikia shilingi milioni 1.8 kwa mwaka

0
5

Makadirio yanaonesha kuwa wastani wa mzigo wa kodi kwa kaya nchini Tanzania umefikia takribani shilingi milioni 1.84 kwa mwaka, sawa na karibu shilingi 154,000 kwa mwezi kwa kuzingatia makadirio ya jumla ya mapato ya kodi ya shilingi trilioni 30.23.

Kwa mujibu wa Tanzania Investment and Consultant Group Ltd, takwimu hizo zinatokana na mgawanyo wa mapato ya kodi kwa takribani kaya milioni 16.4 nchini, kulingana na makadirio ya ukuaji wa idadi ya watu na kaya.

Mzigo wa kodi kwa kila kaya unamaanisha wastani wa kiasi cha kodi kinachochangiwa na kila kaya nchini Tanzania, ikijumuisha kodi za moja kwa moja kama kodi ya mapato ya mtu binafsi na kodi ya majengo, pamoja na kodi zisizo za moja kwa moja, kama VAT na ushuru wa bidhaa unaolipwa kupitia matumizi ya bidhaa na huduma.

Takwimu zinaonesha ukuaji wa idadi ya watu umefikia wastani wa asilimia 3 kwa mwaka, ukiongezeka kutoka watu milioni 61.7 katika Sensa ya mwaka 2022 hadi makadirio ya watu milioni 70.5 mwaka 2025. Kutokana na wastani wa watu 4.3 kwa kila kaya, idadi ya kaya imeongezeka kutoka milioni 14.3 hadi takribani milioni 16.4 katika kipindi hicho.

Wakati huo huo, Pato la Taifa (GDP) la Tanzania linatarajiwa kuongezeka kutoka dola bilioni 79.2 mwaka 2024 hadi dola bilioni 87.4 mwaka 2025, sawa na ukuaji wa asilimia 10.3, unaochangiwa na sekta muhimu kama madini, utalii, kilimo na huduma za kifedha. Serikali pia inatarajia kuongeza uwiano wa mapato ya kodi kwa Pato la Taifa hadi asilimia 13.3, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza ukusanyaji wa mapato pamoja na kuboreshwa kwa ufanisi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ripoti imeeleza kuwa Tanzania inatumia mfumo wa kodi ya ‘Pay As You Earn (PAYE)’ unaopanda kulingana na kiwango cha mapato. Katika mfumo huo, kadiri mapato yanavyoongezeka ndivyo kiwango cha kodi kinavyoongezeka. Mfumo huo hulinda watu wenye kipato cha chini kwa kuwapa kiwango kisichokatwa kodi, huku wale wenye kipato kikubwa wakichangia kodi zaidi kulingana na mapato yao.

Kwa upande wa watu wasiokuwa wakazi wa Tanzania, wao hutozwa kodi ya moja kwa moja ya asilimia 15 kwa mapato yote wanayopata nchini.

Send this to a friend