Wageni wa ndani na nje ya nchi watakaolala kwenye huduma za malazi zilizosajiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii (hoteli, kambi na loji) kwa mujibu wa sheria kuanzia Oktoba 1, 2020 watatakiwa kuanza kusajiliwa kwenye mfumo wa kielektoniki wa MNRT PORTAL.
Lengo kuu la kusajili wageni hao katika huduma hizo ni kupata taarifa zitakazosaidia Serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kuboresha sekta ya Utalii nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga na kueleza kuwa wageni hao watatakiwa kuwa na Vitambulisho vya Taifa (NIDA) au hati za kusafiria na wale ambao hawatakuwa na vitambulisho hivyo watasajiliwa kupitia namba za simu au vitambulisho vya udereva.
Chitaunga amewatoa hofu wamiliki wa malazi kuwa taarifa hizo zitatumika kwa ajili ya matumizi ya serikali pekee na zitatunzwa kwa usiri wa hali ya juu.
Kwa upande wake, Samson Nelsa ambaye ni mmiliki wa huduma za malazi katika Mkoa wa Pwani, amesema mfumo huo utasaidia serikali kuandaa takwimu za idadi ya watalii na wamiliki wa hoteli watakuwa na sehemu salama ya kuhifadhia taarifa zao.