Watalii wa Kenya wakimbilia Tanzania baada ya ada ya kuingia Masai Mara kupandishwa

0
46

Seneta wa Narok nchini Kenya, Ledama Ole Kina, ameeleza nia yake ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga ongezeko jipya la ada ya kuingia Hifadhi ya Masai Mara lililowekwa na gavana wa kaunti hiyo, Patrick Ole Ntutu.

Katika mahojiano yake na chombo kimoja cha habari nchini humo, seneta huyo amelalamika hatua hiyo kufanyika bila kuwashirikisha wadau na umma kabla ya kuongeza viwango vya ada.

“Kama mtu aliye na jukumu la kikatiba la kulinda kaunti, ninatekeleza wajibu wangu kwa kuhakikisha kwamba nafungua kesi mahakamani kuzuia hili kwa sababu kutakuwa na upotezaji mkubwa wa ajira,” amesema.

Seneta amedai kwamba hatua ya serikali ya kuongeza ada bila mazungumzo ya wazi itaweza kusababisha watoa huduma za utalii kupeleka watalii wao kwenye hifadhi nyingine kama Serengeti ya Tanzania au Kruger nchini Afrika Kusini.

Viwango vipya vya ada vimeanza kutumika mwezi huu wa Januari, ambapo sasa watu wazima watatozwa Ksh3,000 [TZS 47,358] na wanafunzi Ksh1,000 [TZS 15,786], tofauti na viwango vya awali vya Ksh1,000 kwa watu wazima na Ksh300 [TZS 4,735] kwa wanafunzi.

Send this to a friend