Watano wafikishwa mahakamani kwa tuhuma za usafirishaji wa bangi

0
10

Watu watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma leo na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi kutokana na tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Washitakiwa hao ambao ni Theddy David (37), Fidelis Marwa (50), Emmanuel Mwamlaga (22), Shabani Rashidi (46), na Anna Bosco (29) ambaye ni kondakta wa basi la kampuni ya New Best Line, walikamatwa wakiwa na magunia 15 ya bangi yenye uzito wa kilo 300.88 katika basi walilokuwa wakisafiria lenye namba za usajili T882 EDS kutoka mkoani Mara kwenda Dar es Salaam.

Wakisoma mashtaka hayo, mawalakili waandamizi wa Serikali, Patricia Mkina na Zubeda Lyaumi wamedai washitakiwa hao walikamatwa Desemba 24, 2024, katika maeneo ya stendi kuu ya mabasi ya Nanenane, mkoani Dodoma, wakiwa na magunia 15 ya ‘sigara kubwa’.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Denis Mpelembwa, amewataka watuhumiwa wasijieleze lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi.

Aidha, watuhumiwa wataendelea kubaki rumande kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana hadi itakapotajwa tena Januari 20 2025.