Watano wakamatwa kwa ubakaji na ulawiti wa watoto Morogoro

0
64

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kutenda makosa ya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo na wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wilayani Malinyi mkoani humo.

Akizungumza Kamanda wa Polisi mkoani humo, Alex Mkama amesema mtuhumiwa wa kwanza, Juma Said (23) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Njiwa anatuhumiwa kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka 13 Aprili 14 mwaka huu.

Mtuhumiwa mwingine ni ni Stanley Mbena (39) mkazi wa Kola ‘A’ Manispaa ya Morogoro anayedaiwa kumlawiti mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa katika tukio lililotokea Mei 3, mwaka huu.

Mkama, alitaja tukio lingine lilitokea Mei 3, mwaka huu ambapo polisi ilimtia mbaroni Tonny Myolele (17) mwanafunzi na mkazi wa Kata ya Ngoherenga Wilaya ya Malinyi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenzake wa shule ya sekondari Ngoheranga mwenye miaka (15).

Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma za ubakaji mwanafunzi ni Iddy Mwanzi (23) mkazi wa Kata ya Kauzeni Manispaa ya Morogoro anayetuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa shule ya Sekondari Kauzeni mwenye miaka 16.

Mtuhumiwa wa mwisho aliyetiwa mbaroni ni Alex Chulongola (34) mkazi wa Kingurunyembe Manispaa ya Morogoro anayetuhumiwa kumbaka mtoto wake mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafuzi wa shule ya Msingi Kigurunyembe Mei 2 mwaka huu.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linaendelea na upelelezi na mara ukikamilika watuhumiwa hao wote watafikishwa mahakamani.