Watanzania watano wafariki kwenye ajali ya moto Afrika Kusini

0
40

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amethibitisha vifo vya Watanzania watano katika ajali ya moto uliozuka kwenye jengo jijini Johannesburg nchini humo.

Balozi Milanzi amesema jengo hilo lilishika moto Agosti 31, mwaka huu, huku walioathiriwa zaidi na moto huo wakiwa ni Watanzania na raia wengine kutoka Malawi na Zimbabwe.

Amesema juhudi za kutafuta miili zinaendelea, lakini mpaka jana idadi iliyotambuliwa ilikuwa 74 wakiwemo raia watano wa Tanzania ambao bado hawajatambuliwa majina na jinsia zao.

“Serikali ilishatangaza jengo lile lisitumike, kwa hiyo wengi waliokuwamo humo hawakuwa na vibali maalumu vya kuishi Afrika Kusini. Waliowatambua wenzao ni Jumuiya ya Watanzania huku Afrika Kusini, sisi tumeshindwa kuwatambua kwa sababu huwa hawafiki ubalozini lakini tunaendelea kuwasaidia,” alisema.

Ameongeza kuwa timu ya maofisa wa ubalozi wa Tanzania ipo eneo la tukio wakiendelea na juhudi za kuwatafuta walioathiriwa na ajali hiyo.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend