Watatu wahukumiwa jela miaka 30 kwa kusafirisha bangi

0
6

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema kwa kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba, 2024 hadi sasa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa ubakaji na usafirishaji dawa za kulevya ambapo watuhumiwa wawili wamehukumiwa kifungo cha maisha na wengine sita wamehukumiwa miaka 30 kila mmoja na mmoja miaka 18.

Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Justine Masejo amesema kupitia operesheni dhidi ya dawa za kulevya, wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 40 wakiwa na mirungi Kilogramu 646.62, na watuhumiwa 25 wakiwa na bangi kilogramu 178.5 pamoja na kuteketeza hekari 16 za bhangi.

SACP Masejo ameongeza kuwa baada ya kufikishwa mahakamani, watuhumiwa watatu wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa makosa ya kusafirisha bangi na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.

Aidha, kwa upande wa makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, amebainisha kuwa wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 51 na kuwafikisha mahakamani, ambapo 20 walikamatwa kwa tuhuma za kubaka na mtuhumiwa mmoja alihukumia kifungo cha maisha, na watuhumiwa wawili walihukumiwa kwenda jela miaka 30, huku wengine kesi zao zikiwa katika hatua mbalimbali.

Kamanda Masejo ameendelea kufafanua kuwa watuhumiwa wengine 31 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ulawiti, ambapo kati yao watuhumiwa wawili wamehukumiwa vifungo vya maisha jela na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.

Send this to a friend