Watatu wakamatwa kwa kumvua nguo na kumuibia mchungaji Kenya

0
44

Polisi jijini Nairobi nchini Kenya wamewakamata watuhumiwa watatu wa wizi wanaodaiwa kumteka mchungaji na kumvua nguo kisha kumuibia Ksh.55,000, sawa na TZS 970,000.

Taarifa kutoka Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kenya (DCI) imefichua kuwa tukio hilo lilitokea wakati mchungaji huyo akielekea kupata chakula cha jioni baada ya kumaliza maandalizi ya kampeni yake ya Benny Hinn itakayofanyika wiki ijayo katika Uwanja wa Nyayo.

Kwa mujibu wa DCI, watatu hao, Bernard Mbunga, Alphonse Munyau, na Samuel Musembi, walimvua nguo mchungaji na kumpiga picha ambazo walitumia kumlazimisha kufuata matakwa yao, wakimtishia kuwa wangechapisha picha hizo za utupu kwenye mitandao ya kijamii.

“Mtu wa Mungu akaamua kushirikiana na watu hao, wakachukua [fedha] kutoka kwenye akaunti yake ya M-Pesa,” imeeleza taarifa ya DCI na kuongeza kuwa mchungaji huyo alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi na kufanikiwa kuwakamata wahusika.

Send this to a friend