Watu watatu wameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kudaiwa kufanya mauaji ya mwanamke aliyejulikana kwa jina la Sagali Masanja (62) mkazi wa Kijiji cha Mahene ambaye alikutwa amekatwakatwa mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na imani za kishirikina.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kukata titi la mwanamke huyo na sehemu za siri kisha kuondoka nazo pamoja na begi la nguo la marehemu, ndipo wananchi wakaanza kuwafuatilia na kufanikiwa kuwakamata watu wawili waliofanya tukio hilo pamoja na mwanamke mmoja ambaye ni mganga wa kienyeji ambaye anadaiwa kuwazindika/ kuwaosha kwa dawa ili wasikamatwe.
Watu hao ni Masumbuko Ngassa (33), Msukuma na mkazi wa Segese wilayani Kahama, Shilinde Kaseko (30) mkazi wa Kijiji cha Seki wilayani Nzega na Sana Maganga (66) Msukuma na mganga wa kienyeji ambaye pia ametajwa kuwa ni Mama mzazi wa mtuhumiwa Kaseko.
“Baada ya Polisi kufika eneo la tukio kutokana na taarifa walizopewa na wananchi, walifanikiwa kufuatilia na kuwakamata watuhumiwa watatu ambao ndio waliowatuma watuhumiwa wawili kwenda kufanya mauaji hayo,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.
Imeeleza kuwa waliokamatwa ni Lucia Mabula (36), Msukuma mkazi wa Mahene ambaye ndiye aliyewatafuta na kuwalipa shilingi laki 2 waliofanya mauaji na chanzo kikiwa ni imani za kishirikina kuwa mwanamke aliyeuawa alikuwa mchawi na kwamba alimroga mtoto wake mwaka 2023, aliyefariki kwa kutumbukia ndani ya kisima.
Mtuhumiwa wa pili ametajwa kuwa ni Makenzi Mabula ambaye ni mume wa Lucia Mabula na wa tatu ni Ramadhani Kurwa wote wakazi wa Mahene.