Wateja TigoPesa wavuna shilingi bilioni 2.7

0
49



Dar es Salaam, 19 Mei 2020: Kampuni inayoongoza kwa mawasiliano ya kidigitali nchini Tanzania, Tigo, leo imetangaza kuwalipa wateja wake wanaotumia huduma ya kifedha ya Tigo Pesa kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kama faida iliyopatikana kwenye robo ya kwanza ya mwaka 2020 iliyoishia tarehe 31 Machi 2020. Hii itakuwa ni mara ya 24 tangu kampuni izindue utaratibu huu wa kutoa gawio kwa wateja wake.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kifedha kupitia simu za mkononi wa Tigo Tanzania, Angelica Pesha, amesema Tigo imewalipa wateja wake wa huduma za kifedha jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 100.9 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu mnamo mwezi Julai 2014.
Pesha amesema, mgao wa robo ya kwanza kwa mwaka huu 2020 unakuja katika kipindi ambacho dunia nzima imeathirika kutokana na janga la COVID-19, na kwamba biashara imekuwa ikizorota kutokana na changamoto za kiuendeshaji hususani katika robo ya kwanza ya mwaka.
“Kufuatia mataifa kuathiriwa na janga la COVID-19 ikiwemo hapa Tanzania, mgao huu unalipwa kwa mteja mmoja mmoja, mawakala wadogo, mawakala wakubwa pamoja na wabia wengine wa kibiashara wanaoshirikiana na Tigo ambao wote watalipwa kwa kuzingatia kiasi cha thamani waliyoweza kuhifadhi kwenye akaunti zao za Tigo Pesa.” Pesha ameeleza.
“Tunajivunia kutangaza ongezeko hili la mgao kwa mara ya 24 mfululizo, tukiamini tunaleta ahueni kwa mamilioni ya watumiaji wa Tigo Pesa hususani katika kipindi hiki kigumu, mgao huu utawasaidia kutimiza baadhi ya mahitaji yao ya kifedha. Na hii, inadhihirisha wazi kwamba Tigo imedhamiria kutoa huduma bora za kifedha kwa wateja wake na nchi nzima kwa ujumla kupitia huduma za Tigo Pesa,” amesema Pesha.
Pesha ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa Tigo imekuwa ikiendelea kupata faida kutokana na ongezeko la watumiaji wa huduma ya Tigo Pesa hususani wa kitengo cha mawakala wakubwa. Tigo Pesa kwa sasa ina jumla ya mawakala wakubwa zaidi ya 50,000 walio katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na mawakala wa kawaida zaidi ya 110,000 wanaowezesha wateja kupata huduma za kifedha kote nchni.
Kwa mujibu wa Pesha, hapo kabla, gawio kwa wateja wa Tigo Pesa lilikuwa linapatikana kwa kuangalia wastani wa kila siku wa kiasi cha fedha kilichohifadhiwa katika akaunti ya mteja na kwamba mgao wa mwaka huu unafanyika kwa kuzingatia mwongozo wa Benki Kuu ya Tanzania uliotolewa mwezi Februari 2014.

####



Send this to a friend