Watoa huduma ndogo za fedha watakiwa kujisajili kabla ya Oktoba 31

0
48

Serikali imewataka watoa huduma ndogo za fedha kujisajili na kukata leseni kabla ya tarehe 31 Oktoba, 2020, kipindi ambacho ni cha mpito kilichowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2019 kabla ya Sheria hiyo kuanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Novemba, 2020.

Rai hiyo imetolewa Mjini Morogoro na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Adolf Ndunguru wakati akifungua mpango wa utoaji elimu kwa umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa wadau wa Sekta hiyo kutoka Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa.

Dkt. Mwamwaja alisema lengo la kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma hao ni kuiwezesha Serikali kuwatambua watoa huduma hao ili kuboresha usimamizi na udhibiti wa Sekta Ndogo ya Fedha nchini na kuwa na Sekta ya Fedha iliyo endelevu na yenye kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa kuwa sekta hiyo ni muhimu katika uchumi wa nchi.

“Sekta hii inatoa huduma za fedha kwa wananchi wa kipato cha chini ambazo zinachangia kuinua uchumi na kuongeza kipato, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya Taifa wanapata huduma za fedha kutoka Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha”, alisisitiza.

Alisema kutokana na umuhimu huo Serikali imekuwa ikitoa elimu ya kuwawezesha wananchi kutekeleza Sheria hiyo na mpango wa utoaji elimu hiyo kuzinduliwa rasmi Desemba, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ambapo sasa elimu hiyo inaendelea kutolewa kwa wadau wa Kanda ya Kati.

Send this to a friend