Watoto chini ya miaka 15 wajihusisha na wizi na ubakaji

0
16

Wananchi wa Kijiji cha Puma Wilaya ya IKungi mkoani Singida wamewalalamikia baadhi ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 katika wilaya hiyo kushiriki katika vitendo vya wizi na ubakaji nyakati za usiku.

Wanakijiji hao wametoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba kusikiliza kero mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Samwel Mdimu amedai walifanya msako na kukamata baadhi ya watoto kisha kuwapeleka kituo cha polisi, “Maofisa wa polisi walishauri watoto hao waachiwe kwa kuwa walikuwa na umri mdogo na kuwataka wazazi wao waelezwe ili waonywe.”

Hata hivyo licha ya wazazi kukiri juu ya vitendo vya watoto wao, wamedai hawana pa kuwapeleka, huku wananchi wakidai vitendo hivyo vimekithiri katika eneo lao hadi kufikia kiwango cha kutokuwa na uhakika wa kuamka salama.

Naye Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ikungi, Suzana Kidiku ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo kufanya msako wa kina na kuwabaini watoto hao wanaotajwa kushiriki vitendo vya wizi na ukabaji na kuwafungulia mashtaka.

Chanzo: Nipashe