Watoto wamzika baba yao mzazi akiwa hai

0
43

Mzee Florence Komba (78) mkazi wa Kijiji cha Mahanje Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, amefariki dunia baada ya kuzikwa akiwa hai na watoto wake wawili kwa tuhuma za kumuua mwanaye Severine Komba (34).

Inadaiwa kuwa, watoto wake kwa kushirikiana na baadhi ya vijana wa kijijini hapo, walimzika kwenye kaburi lililoandaliwa kwa ajili ya maziko ya Severine.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Jabiri Fussi amesema Agosti 11 alipewa taarifa ya Severine kujifungia ndani takribani siku mbili na mara alipofika nyumbani kwa marehemu alikuta mlango umefungwa hivyo kuomba ridhaa ya polisi kuvunja mlango.

“Baada ya kuvunja mlango tulimkuta mtu (Severine) amefariki dunia, tulikaa na familia kufahamu kama kuna mashaka yoyote juu ya kifo hicho, walijibu hakuna mwenye mashaka kwa kuwa marehemu alikuwa anaumwa kwa muda mrefu na alikuwa anaishi pekee yake.”ameeleza.

Ameeleza baada ya kuruhusu maziko yafanyike, alipigiwa simu akiwa ziarani kwamba watoto wa familia hiyo wamemzika baba yao mzazi wakimtuhumu kuhusika na kifo cha ndugu yao kutokana na imani za kishirikina.

“Baada ya kupata taarifa niliwasiliana na polisi waliofika bila kuchelewa. Walienda hadi makaburini, wakaufukua mwili wa mzee huyo na kuutoa ili taratibu zaidi za kisheria zifanyike na kisha tuliuzika upya mwili huo.” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema amekemea kitendo hicho cha kikatili na kwamba hakipaswi kufumbiwa macho hivyo lazima sheria ifuate mkondo wake.

Send this to a friend