Watoto wawili wauawa Mara, chanzo imani ya kishirikina

0
45

Watoto wawili wa familia moja wamefariki katika tukio la mauaji lililotokea Kijiji cha Rung’abure, Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, ambapo chanzo kinadaiwa ni imani za kishirikina.

Watoto hao ni Mwikwabe Saina (10), mwanafunzi wa darasa la tatu, na Joseph Saina (4). Tukio hilo lilitokea Februari 10, 2026 majira ya saa 11 alfajiri katika Kitongoji cha Getasamo, Kata ya Rung’abure.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, watoto hao walishambuliwa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali, huku mtuhumiwa akitajwa kuwa Joseph Marwa (18), mkazi wa eneo hilo.

Uchunguzi wa awali umeeleza kuwa mtuhumiwa alimtuhumu mama wa watoto hao kujihusisha na vitendo vya kishirikina, akidai anawaloga ndugu zake.

Baada ya tukio, wananchi walimkamata mtuhumiwa na kuanza kumshambulia kwa fimbo na mawe kabla ya kuokolewa na Polisi. Alipata majeraha makubwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Nyerere (DDH) Mugumu kwa matibabu, ambako alifariki dunia.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kina na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika.

Send this to a friend