
Mahakama nchini China imewahukumu kifo watu 11 kati ya 39 wa familia moja kwa kuendesha vituo vya uhalifu nchini Myanmar, ikiwemo biashara haramu ya dawa za kulevya, kamari, ukahaba, mauaji na kuumiza watu makusudi.
Wanafamilia wengine 11 wamehukumiwa kifungo cha maisha, na wengine wamehukumiwa vifungo vya kati ya miaka 5 hadi miaka 24 pamoja na kutaifishwa kwa baadhi ya mali zao.
Mahakama ya Kati ya Wenzhou katika mkoa wa Zhejiang, imesema kundi hilo liliunda kikundi cha silaha katika Mkoa wa Kokang, Myanmar, na kufanya uhalifu tangu mwaka 2015.
Aidha, taarifa zinaeleza kuwa pesa walizopata kutokana na kamari na utapeli wa simu zilifikia zaidi ya yuan bilioni 10 [TZS Trilioni 3.4].








